Kati ya mamia ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya maarufu Tanzania, ni mwanamuziki mmoja pekee aliyehudhuria katika Tamasha la Sauti za Busara 2014, lililotajwa na Kituo cha Utangazaji cha CNN kuwa ni tamasha lenye nguvu barani Afrika.
Huyu siyo mwingine bali ni Fareed Kubanda (Fid Q), aliyekuwapo mjini
Zanzibar kwa siku mbili kushuhudia tamasha hilo lililokuwa la siku nne,
lililofanyika katika wiki ya pili ya Februari mwaka huu, Viwanja vya
Ngome Kongwe visiwani humo.
Ikumbukwe kuwa Fid Q alianza shughuli za muziki miaka ya 1990. Alitoa
wimbo wake wa kwanza mwaka 2000 ulioitwa; Huyu na Yule, alioimba na Mr
Paul. Wimbo huu ulirekodiwa na Prodyuza maarufu nchini, Master Jay
katika Studio za MJ Records na kumpa heshima kubwa msanii huyo.Azimio la habari lili fanya mahojiano na Fid Q ambaye pamoja na mambo mengine aliweka wazi sababu za yeye kuwapo katika tamasha hilo, kilichomvutia huku akiweka wazi kuhusu biashara ya madini aliyodaiwa kuanza kuifanya mwishoni mwa mwaka jana.
Swali: Nini kimekuvutia ukaamua kuhudhuria katika tamasha hili?
Fid Q: Mimi ni mtu ninayependa kujifunza zaidi,
nimeona hili ni tamasha kubwa na zuri kwangu kujifunza. Kubwa zaidi ni
kutaka kujua wenzetu wanafanyaje muziki. Huwezi kukaa tu na kwenda
kupiga muziki staili moja kila siku; ili ujue, ni vyema ukajifunza
kutoka kwa watu unaowaamini.
Swali: Kupitia wanamuziki wa muziki wa asili kutoka
mataifa mbalimbali katika Sauti za Busara, unadhani unaweza kupata
uzoefu wa kutosha?
Fid Q: Wasanii wote wa mataifa mbalimbali
waliofanikiwa hasa Nigeria, wamekuwa wakichukua vionjo kutoka katika
muziki wa asili, kisha wakileta katika muziki wa kizazi kipya,
inapatikana ladha ya kipekee, ndiyo maana leo unawaona kina P Square
wanatamba, walianza kujifunza na kutumia vionjo kutoka katika muziki wa
asili.
Swali: Unadhani nini kinachowafanya wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutohudhuria tamasha hili?
Fid Q: Hawapo tayari kujifunza. Mimi nimewahi
kutumbuiza katika tamasha hili, ninajua. Huku hakuna ubabaishaji, msanii
unatakiwa uimbe kwa sauti yako jukwaani, walio wengi hili hawaliwezi.
Idadi kubwa ya wasanii wamezoea kuimba kwa ‘playback’, (kuweka cd ya
ala), ndiyo maana hata waandaaji wanashindwa kuwaalika, muziki
tunaofanya sisi ni ule wa wenzetu, lakini tunashindwa kuuwakilisha
ipasavyo, tumezoea kuimba kwa ‘playback’.
Swali: Unadhani kuna umuhimu gani kwa wasanii kuimba ‘live’ (kwa sauti zao wenyewe pasipo kutegemea CD)?
Fid Q: Ina faida zake. Kwanza inakutangaza na pia
unaonekana wewe ni msanii halisi. Haya ndiyo wanayohitaji kuyaona watu
wanaoujua muziki, watu wanaohudhuria matamasha ya kimataifa ni wengi,
hawawezi kusikiliza kitu walichokisikia kwao, wanapenda kusikia kitu
kipya kitakachowateka.
0 comments:
Post a Comment