Sunday, March 16, 2014

2:57 AM


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jana mkoani Iringa (hawako pichani) kuhusu uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga unaofanyika leo. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid. Picha na Edwin Mjwahuzi  


Kalenga. Uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kalenga, Iringa unafanyika leo huku kukiwa na masuala yenye utata ambayo huenda yakasababisha malalamiko baada ya matokeo kutangazwa.
Vyama vitatu; CCM, Chadema na Chausta vimesimamisha wagombea wake katika uchaguzi huo unaotokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, pia Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Hata hivyo, ni wagombea wa Chadema, Grace Tendenga na wa CCM, Godfrey Mgimwa ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda, huku mgombea wa Chausta, Richard Minja akipewa nafasi ndogo kutokana na maandalizi hafifu ya ushiriki wake.
Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Kalenga, Prudenciana Kisaka alisema maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika na kwamba matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa mapema kadri iwezekanavyo ikiwa mambo yatakwenda kama yalivyopangwa.
Jana viongozi wa juu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji Mstaafu Damian Lubuva walikutana na waandishi wa habari, mkutano ambao uliibua mambo kadhaa yenye utata, huku viongozi hao wakishindwa kuyatolea majibu ya moja kwa moja.
Masuala hayo ni uamuzi wa Chadema kutumia chopa wakati wa kutembelea vituo vya kupigia kura, pia suala la masahihisho yaliyofanywa kwenye daftari la kudumu la wapigakura, hivyo kuzua malalamiko mengi kutoka Chadema.
Mmoja wa Makamishna wa NEC, Jaji John Mkwawa alisema kilichofanyika katika daftari hilo ni kurekebisha kasoro ambazo ziliruhusu watu saba ambao waliandikishwa 2010 kuweza kupiga kura. Jaji Mkwawa alitetea uamuzi huo akisema kuwa umefanywa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na kanuni zake.
Kwa upande wake Jaji Lubuva alisema: “Kimsingi hakuna jina lililoongezwa wala kupunguzwa kwa sababu kilichofanyika siyo maboresho makubwa ya daftari, bali ni masahihisho.”
”Ufafanuzi wa NEC unatokana na malalamiko yaliyotolewa na Chadema kwamba marekebisho yaliyofanywa yameongeza watu zaidi ya 1000 wapya katika daftari hilo kinyume na sheria.
Upigaji wa kura:
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, vituo vya kupigia kura vitakuwa wazi kuanzia saa 1 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni, ambapo watu 71, 765 wamejiandikisha Jimbo la Kalenga.

0 comments:

Post a Comment