Tuesday, March 18, 2014

12:16 AM

“‘Short time’ vipi? Ni Sh.10,000 tu, gharama ya chumba kwangu.” Hivi ndivyo nilivyopokelewa na binti wa miaka 21 katika Mtaa wa Uhindini mkoani Dodoma nilikokwenda saa 4 usiku kufuatilia taarifa za kinadada wanaofanya biashara haramu ya ngono, maarufu kama changudoa.

Uhindini ni mtaa maarufu mkoani Dodoma kwa biashara ya ngono, ikifuatiwa na maeneo mengine kama Chako ni Chako, Mwanga Bar na zaidi, katika kumbi za starehe kama Club 84 na Maisha.
Wakati nazungumza na binti huyo mfupi na maji ya kunde, kinadada wengine kadhaa, walikuwa wakitufuatilia kwa karibu kuona kama tumekubaliana au tumeshindwana bei ili na wao wataje gharama zao.  

“Sh.8,000 huduma ya chapchap (short time) chumbani, Sh.5000 hapa hapa na Sh.70,000 saa 5:00 (usiku) mpaka asubuhi,” walijinadi wengine wakijaribu kile wanachokiita bahati yao.  

Hata hivyo, baada ya kugundua kuwa sikuwa na lengo la kufanya nao biashara, wote walirudi nyuma kusubiri wateja wengine. Ndipo nilipomwita binti huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Monica na kufanya naye mazungumzo kama ifuatavyo;  

Mwananchi: Habari yako binti? Mimi niko hapa kikazi na ningeomba nichukue dakika zako kadhaa ambazo nitazilipia kwa Sh.10,000. Nilitamani kujua kazi hiyo ulianza lini na nini kilikusukuma kuifanya?  

Monica: Ni hadithi ndefu. Nilianza kuifanya mwaka juzi nikiwa na umri wa miaka 19. Nililazimika kuifanya baada ya baba yangu wa kambo kuonyesha kutokunijali kabisa na nikahisi sina thamani kwenye familia yake.  

Mwananchi: Wewe ni mwenyeji wa wapi na wateja wako ni kina nani hasa?  

Monica: Mimi ni mtu wa Singida, naifanya biashara hiyo sanasana hapa Dodoma wakati wa Bunge. Baada ya hapo narudi kuendelea nayo huko huko Singida.  

Mwananchi: Unatumia vigezo gani kupanga gharama za huduma zako?  

Monica: Inategemea nazungumza na mtu mwenye mwonekano gani. Gharama ya short time kwa mtu wa hali ya juu inaanzia Sh.20,000 na kulala ni Sh.100,000 hapa malipo ya chumba kwangu. Kwa mtu wa kawaida naanzia Sh.5000 short time hadi Sh.20,000 hii hakuna kulala.  

Mama mtu mzima anayekadiriwa kuwa na kati ya umri wa miaka 40 na 50 ambaye hakutaka kutaja jina lake, anaeleza kuwa biashara ya ngono imemsaidia katika mambo mengi, ikiwamo kuwasomesha watoto wake wawili; mmoja chuo kikuu na mwingine kidato cha nne.  

“Hakuna biashara inayonilipa kama hii. Nimesomesha watoto wangu, nalipa kodi ya pango na kuishi mjini kwa kazi hii,” anasema.  

Alipotakiwa kueleza kulichomsukuma kuifanya kazi hiyo alijibu, “Mwaka 2008 niliamua kuachana na mume wangu wa ndoa baada ya mateso na manyanyaso makubwa niliyoyavumilia kwa miaka mingi. Kwa kuwa sikuwa na namna ya kukidhi mahitaji yangu, nikajiingiza kwenye biashara hiyo ambayo naona inanilipa.



Mmoja wa madereva wa bodaboda wanaosubiri abiria eneo hilo, anaeleza kuwa mmoja wa kinadada hao ni mteja wake mkubwa. Anaingia kazini saa 12:30 na anatoka saa 4:30, anasema na kuendelea; 

“Kwa muda huo tu hakosi Sh.50,000 ndiyo maana hawataki kuchukuliwa kwa makubaliano ya kulala. Kama unavyoona, mashangingi yanavyopaki na kuondoka, wana wateja hasa katika siku hizo za Bunge.”
 

Ukikaa eneo hilo kwa muda, utagundua kwamba kuna nyumba mbili za kulala wageni (majina tunayo), wanazotumia kinadada hao kuwaingiza wateja wao kwa makubaliano maalumu.
 

Mhudumu katika moja ya nyumba hizo amesema “Sitaki hata mteja wa kuja kulala hapa, malipo ninayopata kutoka kwa kinadada hao yanatosha.”
 

Mhudumu huyo anaeleza kuwa kwa kila chumba kinachotumiwa kwa short time, anapata Sh.4000 pesa ambayo inalipwa na mwanadada anayemwingiza mteja wake.
 

“Na hii inachukua siyo zaidi ya dakika kumi. Kwa mtindo huo, unaweza ukatengeneza hata Sh.200,000 kwa siku, sasa mimi mteja wa kulala wa nini?” alihoji.
 

Wakati tukifanya mazungumzo hayo, magari yalikuwa yakisubiri kwa foleni nje ya nyumba hizo, huku watu wakionekana kuingia na kutoka wakipishana siyo zaidi ya nusu saa.
 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime anasema anafahamu tatizo hilo na tayari tumekuwa tukilifuatilia kwa karibu kulimaliza.
 

“Tumekuwa tukitoa taarifa mara kadhaa kuhusu suala hilo, tunaendelea kulifuatilia kwa karibu,” anasema kwa kifupi.

Spika Makinda atahadharisha wajumbe.


Siku chache baada ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwasili Dodoma, Spika wa Bunge Anne Makinda alizungumza na wajumbe wanawake bila kumung’unya maneno anasema, “Jihadharini na Ukimwi Dodoma.”

  Spika Makinda anawaeleza wajumbe hao kuwa wanapaswa kujiheshimu ili wamalize kazi iliyowapeleka Dodoma kwa salama badala ya kujiingiza kwenye mambo ambayo yatahatarisha maisha yao. 

“Mtu unalewa mpaka hujitambui na baadaye unabebwa na wanaume, unadhani wanakupeleka wapi?” anahoji.

0 comments:

Post a Comment