Tuesday, March 4, 2014

9:58 AM

 

Afisa wa Polisi Amtwanga RISASI Mkewe, Kisha Ajiua

AFISA wa Jeshi la Polisi nchini Kenya amemjeruhi vibaya mkewe kabla hajajiua. Tukio hilo lilijiri majira ya saa saba unusu usiku ndani ya makazi yao huko South B, Nairobi.
Gazeti la Daily Nation la nchini humo limeripoti kuwa, kabla ya tukio hilo askari huyo mwenye cheo cha Sajini Mwandamizi katika ofisi za Westlands, alirejea nyumbani usiku wa manane na kuanza ugomvi na mkewe. Taarifa zinaeleza kuwa ugomvi huo ulihusu kodi ya pango walilokuwa wakiishi.
Sajini Mwandamizi huyo alimdai mkewe kiasi cha shilingi za Kenya 16,000 alizokuwa amempa kabla kwa ajili ya kulipia pango kwa mwezi huu Machi. Hata hivyo, mkewe hakuweza kutoa kiasi hicho cha pesa wala kuwa na maelezo yaliyotosheleza.
Kwa mujibu wa jirani yao, Peter Thuita, kulisikika yowe zilizofuatiwa na mlio wa risasi majira ya saa tisa usiku kutoka nyumbani kwa afisa huyo wa polisi.
Mkuu wa Upelelezi eneo la Makadara, Zach Nanguli amesema kuwa afisa wake huyo alirejea nyumbani mapema isivyo kawaida lakini akiwa tayari ameutwika kiasi cha kutosha. Kisha, akamtwanga mkewe risasi tano ikiwa ni shingoni, mguuni, mkononi, begani na tumboni kabla mwanamke huyo hajafanikiwa kujinusuru kwa kukimbilia nje ya nyumba hiyo. Baada ya hapo, afisa huyo akajitwanga risasi kichwani na kufariki papo hapo.
Mwanamke huyo anayefahamika kwa jinala Janet Atieno, alikimbizwa hospitalini Mariakani akiwa mahututi. Mwanamke huyo pia ni afisa wa polisi akiwa na cheo cha Konstebo akihusika zaidi na ulinzi wa majengo ya serikali katika eneo la Uhuru.
Silaha ya Sajini Mwandamizi, bastola ikiwa na risasi saba ilipatikana katika eneo la tukio. Afisa Upelelezi amesema pia walikuta maganda nane ya risasi zilizotumika.
Afisa huyo aliyejiua aliandika katika ukurasa wake wa Facebook muda mfupi kabla ya zahma hiyo. Aliandika;
“Lazima nifanye jambo la kijinga. Liwe liwalo. Nimechoka”.

 

0 comments:

Post a Comment