Ni takriban miaka 10 sasa tangu kuanzishwa kwa shule za kata hapa nchini kupitia mpango kabambe uitwao “Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES). Msisitizo mkubwa uliwekwa na Serikali kuhakikisha majengo yanajengwa hata kama hakuna mwanafunzi.
Kubwa zaidi ilikuwa ni kampeni ya kuhamasisha jamii pana kuzipokea
shule hizo na kuamini kuwa ndiyo mkombozi wa wanyonge. Yaani hakuna haja
ya kupeleka mtoto nje ya vijiji au kata zao, kwa kuwa shule za kata
zinatosha kuwakomboa. Kwa Watanzania wengi hasa wale wa maeneo ya
vijijini, uamuzi huu ulikuwa ni pambazuko jema.
Hata hivyo, watafiti na wapenda maendeleo walikosoa mapema ujenzi wa
pupa wa shule za kata bila ya kuwepo kwa mkakati maalumu wa kuziwezesha
kuwa na manufaa yanayotarajiwa. Watafiti na wanaharakati hawakueleweka
machoni pa Serikali na baadhi ya wana jamii. Walionekana kama wahaini
ama wapinga maendeleo.
Hoja kubwa kwa watawala ilikuwa ni kwamba shule hizo zipewe muda na
kwamba baada ya miaka michache kila kitu kitakamilika na elimu itaboreka
na Watanzania watanufaika. Kweli tukazipatia muda wa kutosha sasa ni
miaka 10. Ubora wa elimu kwenye shule hizo unasikitisha.
Mwaka 2010 wanafunzi waliopata daraja sifuri na daraja la nne
walikuwa asilimia 88. Mwaka 2011 walikuwa asilimia 90.2. Mwaka 2012
wakafeli asilimia 87 huku waliopata daraja sifuri wakiongezeka hadi
asilimia 60.
Mwaka 2013 katika matokeo yaliyotoka hivi karibuni, waliopata sifuri
na daraja la nne ni asilimia 80. Waliopata sifuri pekee ni asilimia 42.
Kwa uchambuzi wa kina kama kusingepangwa madaraja kwa mfumo mpya, sifuri
zingeongezeka hadi asilimia 70.
Baadhi ya shule tangu kuanzishwa kwake hazijawahi kushuhudia
mwanafunzi hata mmoja akipata daraja la kwanza au la pili. Na baadhi
hazijawahi kushuhudia mwanafunzi hata mmoja akipata daraja la tatu.
Kinachoshangaza hata shule zilizonadiwa kwa majina ya viongozi
hazipewi msaada wowote hata wa hamasa na viongozi hao. Watoto
wanaendelea kukusanya ziro kila mwaka.
Mfano ni shule kama Sekondari ya Lowasa, ambayo wanafunzi waliopata
sifuri ni wanafunzi 71 kati ya wanafunzi 179, waliobahatika kupata
daraja la kwanza ni 2 tu. Katika Sekondari ya Yusufu Makamba, waliopata
ziro ni 112 kati ya wanafunzi 310, hakuna hata mmoja aliyepata daraja la
kwanza japo shule hii iko jijini Dar es Salaam kwenye kila kitu.
Shule ya Sekondari ya Anna Mkapa kulikuwa na ziro 72 kati ya
wanafunzi 192. Waliopata daraja la kwanza ni wawili tu. Pius Msekwa,
sifuri ni 42 kati ya wanafunzi 124, hakuna hata mmoja aliyepata daraja
la kwanza.
Sekondari ya Jakaya Kikwete, sifuri zilikuwa 43 kati ya wanafunzi
115, daraja la kwanza ni wawili tu. Sekondari ya John Malecelea ziro 15
kati ya wanafunzi 28, hakuna daraja la kwanza.
Hizi ndizo shule zenye majina ya vigogo. Hali inatisha. Tuendelee
kuzipa muda hadi lini? Hali inadorora kila kukicha. Baadhi zilianza na
walimu kadhaa sasa hazina walimu, na waliopo wamekata tamaa; hawajitumi
kabisa.
Miaka 10 ni mingi. Kama kweli kuna nia ya kuboresha elimu hasa za
mikoa masikini iliyotengwa tangu historia tungeona maendeleo. Ziko shule
binafsi zinazoanzishwa ndani ya miaka miwili shule na mafanikio
yanakuwa makubwa kitaifa.
Nikumbushe tu kuwa wanafunzi wanaopata sifuri katika shule za kata
siyo kwamba hawana akili. Mfumo umewafelisha hata kabla hawajaanza
shule. Nani asiyejua shule nyingi za kata zina upungufu mkubwa wa
walimu? Baadhi ya shule zina walimu wawili tu au mmoja.
Isitoshe, shule nyingi za kata zinapokea watoto kutoka shule za
msingi za Serikali ambazo wanafunzi wanafundishwa kwa Kiswahili masomo
yote. Lakini, wanapoingia sekondari wanakutana na lugha ngeni na
kutungiwa mitihani kwa lugha hiyo.
Wanatungiwa mitihani kwa lugha wasiyoielewa wao wala walimu wao, huku
wakishindanishwa na wenzao waliosoma kwa lugha hiyo tangu chekechea.
Hakuna kiongozi asiyejua haya ndiyo maana huwezi kukuta mtoto wa
kiongozi anasoma shule ya kata, japo wanazipigia debe shule hizo kwenye
majukwaa.
Kwa bahati mbaya watawala wanasahau kuwa asilimia tano ya wasomi
wanaofaulu vizuri hawawezi kubeba asilimia 95 ya watu wasiosoma.
Tunajidanganya. Maendeleo ya nchi huendelezwa na jamii kubwa yenye nguvu ya kuzalisha kutokana na kuwa na maarifa.
Wachache hata wakisoma vipi hawawezi kubeba wanajamii wengi.
Watashika vyeo ofisini, watakuwa watawala wanyonyaji bila kuwa na
ubunifu wala uzalishaji wowote.
Narudia kusema: Wanyonge Watashinda! Nguvu ya haki na utu kamwe
haishindwi na fikra za uzandiki na udhalimu. Historia inathibitisha kuwa
dhuluma ina uhai mfupi, huzaa fedheha ya milele na matunda ya haki
hudumu na kutamalaki daima. Yanakuja!
MWANANCHI
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment