Serengeti. “Ni zaidi ya miezi sita tangu nifanyiwe ukatili na mume wangu na mama mkwe. Nahangaika kuuguza mguu niliokatwa kwa panga kunyunyiziwa maji ya betri. sijui kama utapona. Kichanga nacho kinasumbua, jamani nimekosa nini mimi kwa Mungu.”Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio. Maneno ya ya Anna Sabai (20) mkazi wa Kitongoji cha Manyata Kijiji cha Nyamakendo Kata ya Mbalibali, wilayani Serengeti, ambaye anapaza sauti kutaka kujua walipo wanaharakati ambao kwa hali aliyonayo , angeweza kupata msaada kutoka kwao.Ukatili aliofanyiwa Anna, mama wa watoto wawili katika ndoa yake na Hamisi Sabai (20) yenye migogoro na ambayo inazidi kuuweka Mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya kutokana na uwingi wa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.
Agosti Mosi, 2013 ikiwa ni siku ambayo wakazi wa wilaya hiyo
humiminika mnadani, Anna akiwa na uja uzito wa miezi tisa na akihesabu
siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na mume wake kwenda kuchunga
ng’ombe, bila kujali hali yake.
“Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana,” anakumbuka Anna wakati
anaongea na Mwananchi kuhusu ukatili dhidi yake. “Nikiwa malishoni
nilikaa chini ya kivuli huku ng’ombe wakiendelea kula majani. Hali
ilivyozidi kuwa mbaya nilisinzia. Alipokuja mume wangu akanikuta
nimelala na hapo hapo akaanza kunishambulia kwa kipigo, akidai kuwa
nilikuwa na mwanamume kutokana na mapenzi kunoga ndio maana nilisinzia
na kuacha ng’ombe wanazagaa.”
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake, walipofika
nyumbani mama mkwe wake Bhoke Sabai alizidi kumtia hasira kijana wake
akidai kuwa nilikuwa na mwanaume, natakiwa kupewa kipigo ili iwe
fundisho.
“Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea, bado akaona
aache fimbo na akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto,” anasema
Anna huku akitokwa na machozi.
“Niliumia sana… nikatamani kufa, maana hali ilikuwa mbaya. Sikuwa
na msaada. Baadaye akanifungia ndani ili watu wasijue; wala hakuna
kwenda kutibiwa.”
Amwagiwa tindikali ili kuzuia damu isitoke
Huku akiwa amebeba mtoto wake na kutembea kwa shida, Anna anasema
ili watu wasijue unyama aliotendewa, walileta maji ya betri na kumwagia
kwenye kidonda.
“Maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua. Nilifikia hatua
kama ningepata kitu cha kujimaliza, ningejiua. Nilikuwa nasumbuliwa na
mimba na huku naumizwa hivi,” analalamika. “Jamani wanaharakati
wanaotetea wanawake wako wapi maana nitakatwa mguu hivi hivi.”
Anasema matokeo yake mguu ukaoza kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu
na kwamba ndugu zake hawakuambiwa na mama mkwe wake alikuwa akiendelea
kumkejeli kila wakati.
“Sijaona watu wenye roho ya kikatili kama hao, kwa kuwa walilenga kuniua bila kosa,” anasema.
Aokolewa na mama yake mzazi
Anasema kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani
ili majirani wasijue, kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu, kwa nini
afe bila ndugu zake kumwona. Ndipo bila kutarajia alishtukia mama yake
mzazi, Mnanka Chacha (48) akifika hapo baada ya kutaarifiwa na majirani.
“Nilipomwona mama nikasema basi sasa hata kama nikifa, niko katika
mikono salama kwa kuwa huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu.
Nilijua kama ningefia mkononi mwa hao huenda maiti ingetupwa kama mbwa.
Nilijisikia ahueni kwa kumuona mama,” anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu
Anasema kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha Hospitali Teule ya
Nyerere kwa ajili ya matibabu na madaktari walipomwona walimwambia kuwa
hawana uwezo tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo. Hivyo wakamwandikia
barua kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.
Akosa pesa
Kutokana na ukata wake, alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi
nyumbani kwake kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema, ili aweze kwenda
naye Mwanza kwa ajili ya matibabu.
0 comments:
Post a Comment