Sheikh wa Msikiti Mkuu wa Bondeni mkoani Arusha, Mustaph Kiago (49)
na mwanaye Khalid Mustapha (10), wamemwagiwa kimiminika kinachodhaniwa
kuwa ni tindikali wakati wakiingia msikitini.
Sheikh Kiago amejeruhiwa shingoni na mtoto wake ameumizwa machoni na wote wanatibiwa hospitali ya mkoa ya ya Mount Meru
Akizungumza nasi nje ya wodi ya watoto kwenye hospitali hiyo jana,
Kiago alisema amemwagiwa tindikali hiyo jana saa 11.10 alfajiri wakati
anashuka ngazi kuingia msikitini kuongoza sala ya alfajiri.
“Nilipomaliza ngazi ili niiingie msikitini nilimwona kijana nyuma
yangu ameshika kopo lenye maji mekundu na ghafla alinimwagia usoni na
mengine yalimpata mtoto wangu”, alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alikimbia baada ya kuwajeruhi akitumia pikipiki iliyokuwa nje ya msikiti.
Aliendelea kusema kuwa baada ya mtu huyo kukimbia, alirudi ndani na
kumchukua mtoto wake hadi hospitali ya Mkoa Maunt Meru na kugundua kuwa
ameumia macho wakati yeye alichunika ngozi ya shingo na usoni.
Mustapha aliyekuja nchini hivi karibuni akitokea Misri, alisema
ameumia macho na kwamba ana wasiwasi jicho la kushoto halitaona tena.
Sheikh huyo alisema chanzo cha tukio hilo ni vita iliyoanza muda
mrefu ambapo, Februari 7 mwaka huu, akiwa msikitini, alifuatwa na Sheikh
wa Mwanza (jina linahifadhiwa), akiwa na watu kadhaa na kutakiwa
kutangaza jihad misikiti yote ya Arusha.
Alifafanua kuwa alikataa kutangaza jihad ambayo ni vita ya silaha dhidi ya Waislamu na wasio Waislamu akisema;“Nilipinga kwa sababu hatuwezi kuvunja amani tulionayo kwa masuala ya dini, wakaniambia lazima wataniua,”alisema.
Alifafanua kuwa alipowapinga ikatokea vurugu kubwa pale msikitini
ambapo miongoni mwa kundi hilo lililoongozwa na Sheikh wa Mwanza
aliyemtaja (jina tunalo), alimrukia na kumpokonya kipaza sauti lakini
naye akakimbilia kuzima umeme.
Alisema waumini waliokuwepo walituliza ghasia naye alikwenda kutoa taarifa polisi.
Alilalamika kuwa licha ya kufika asubuhi hospitalini mtoto wake hajapata kitanda hivyo alikuwa anamshughulikia kwanza mwanae.
Mtoto Khalid anayesoma darasa la tatu nchini Misri, hakuzungumza kwa kuwa hafahamu Kiswahili na anazungumza Kiarabu.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Japhet Lusingu,
akizungumzia tukio hilo, alisema polisi ina taarifa zake na inaendelea
na uchunguzi.
Alisema mara baada ya tukio hilo, polisi ilijulishwa na kufika eneo
la tukio na kufanya mahojiano na mashuhuda kisha kuchukua kopo
linalosadikiwa kuwa lilikuwa na tindikali hiyo.
0 comments:
Post a Comment