Saturday, March 15, 2014

3:03 AM
WANAWAKE wawili Jumatatu walizuiliwa kwa saa 3 na mahakama moja nchini Uganda kwa kuingia mahakamani wakiwa wamevalia ‘Mini Skirt’.

Hii ni baada ya jaji aliyekuwa mahakamani humo kusema kuwa wanawake hao walikuwa wamevalia nguo zisizofaa.

Kwa mujibu wa taarifa kwenye mtandao wa Daily Nation, nchini Kenya, Bi Prosy Nasuna aliyekuwa amemshitaki Bi Jane Nabukenya kwa kukosa kumlipa deni lake la shilingi milioni 3 za Uganda wote walisemekana kutovalia nguo za heshima na kutatiza kikao cha mahakama.

Walipoingia mahakamani katika eneo la Bukomansimbi wiki jana Prosy pamoja na mshitakiwa walijikuta matatani.
Kabla ya kuchukuliwa hatua kwa mavazi yao, watu walipiga mayowe mahakamani humo wakisema kuwa wawili hao walikuwa wamevalia visivyo kulingana na sheria iliyopitishwa mwezi jana kuhusiana na kupiga marufuku mavazi fupi.

Sheria hiyo inasema kuwa yeyote atakeyeonyesha sehemu za siri za mwili wake hadharani na kusababisha hisia fulani miongoni mwa watu, anakuwa amekiuka sheria.

Minong’ono na kelele za watu zilisababisha hakimu kuamuru kukamatwa kwao kwa kwenda kinyume na sheria na pia kwa kuhujumu mahakama.

Alisema kuwa kesi ilikosa kuendelea kutokana na mavazi yao na kwa hivyo kosa lao lilikuwa kusababisha usumbufu mahakamani kwa kuvalia ‘Mini Skirt’.

Hakimu aliwahukumu jela masaa 3 wanawake hao na kuahirisha kesi yao hadi tarehe 13 mwezi Machi.

0 comments:

Post a Comment