Saturday, March 8, 2014

9:45 PM
Mambo yanazidi kuwa matamu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, ambapo leo asubuhi helkopta ya Chadema iliuteka mji wa Iringa kwa kurusha vipeperushi vya mgombea wao Grace Tendega, katika maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa hasa katika stendi kuu ya mabasi na zingine zilitua Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Iringa.
Kwa mujibu wa shuhuda ambaye ofisi yake ipo mkabala na Ofisi za CCM, alisema kuwa majira ya saa nne leo asubuhi waliona helkopta ya Chadema ikipita kwa chini karibu na majengo huku ikidondosha vipeperushi katika maeneo hayo.
“Mimi na wenzangu tulishituka na kutoka nje kuiona helkopta hiyo, kwanza tulidhani inatua lakini haikuwa hivyo. tuliona ikirusha vipeperushi ambavyo vingine vilitua jengo la CCM, baada ya hapo ikapaa zaidi angani na kuelekea upande wa kusini mwa Mji wa Iringa,” alisema dada huyo.
Chadema ilitangaza kwamba leo inaanza kampeni katika Jimbo la Kalenga kwa kutumia helkopta maarufu kama Chopa, na wangeanzia Kijiji cha Wangama alikozaliwa mgombea wao Grace Tendega.

0 comments:

Post a Comment