Kwa kawaida uvaaji wa mavazi hutegemea hali ya hewa au majira ya husika ya mwaka. Ni muhimu kuzingatia majira ili kuepuka shida au kukosa raha kwa kuchagua vazi lisilo sahihi.
Majira ya joto watu wengi hupata shida ya kuchagua mavazi, kwani
kipindi hicho huwa ni vigumu kwao kuvaa vizuri waendapo kazini au kutoka
kwa ajili biashara au shughuli zao nyingine.
Hata hivyo, kabla hujachagua kuvaa nguo, hata kama ofisi yako ina
utaratibu wa mavazi rasmi ya wakati wa joto, kumbuka mavazi yako yana
nafasi kubwa kwa mwonekano wako na hali ya joto haiwezi kukubadilisha.
Kumbuka kuwa huna sababu ya kuvaa nguo zisizofaa ili kuepuka joto. Siku
zote jiamini na hakikisha unapambana na joto ukilenga kuonekana nadhifu.
Ufuatao ni mwongozo, ambao ukiufuata utakuwezesha kufikia malengo
yako ya kuonekana nadhifu kipindi cha joto, kwani ukifanikiwa kuufuata
vizuri, utaonekana mwenye kujua maana halisi ya mitindo.
Unachotakiwa kufanya
* Vaa nguo zenye tabaka mbili, hii itakurahisishia kubadilisha
kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa. Hapa unaweza kuvaa blauzi yenye
mikono mifupi au ‘top’ na jaketi jepesi ‘blazer’ au koti. Hii
itakurahisishia kuweza kulivua jaketi hilo au koti ikiwa utasikia joto.
unaweza kuvua jaketi au koti lako na kubakia na blauzi au ‘top’.
* Jaribu kuvaa sketi badala ya suruali, hata kama unapendelea kuvaa
suruali, kwani sketi huruhusu hewa kuzunguka katikati ya mapaja na
kuondoa hali ya joto.
* Ili kuepusha usumbufu, hakikisha nywele zako hazikugusi, hivyo ni
vizuri ukazibana kwa mtindo utakaofanya zisiguse shingo yako. Unaweza
kuzikusanya katikati na kuzibana au kuzisuka. Staili hizi zitafanya
nywele zako zisikuguse shingo.
* Paka vipodozi vilivyo angavu, hasa ukiwa nje kwenye joto kali. Joto
kali na vipodozi vingi haviendani. Joto husababisha vipodozi kuyeyuka
na kuondoka, pia husababisha vitundu vya hewa kuziba na ngozi kupasuka.
*Jipake manukato mazuri yanayoendana na majira ya joto. Manukato yenye harufu kali hunukia vibaya kwenye joto.
* Mavazi huendana na vitu vingine kama pochi, viatu, mkanda, hata
herein au mkufu. Unashauriwa kubeba pochi na kuvaa viatu vyenye rangi
angavu.
Usichotakiwa kufanya
* Usivae ‘top’ isiyo na mikono kazini, hata kama una mikono mizuri.
* Usivae kaptula au sketi fupi, labda kama ni sare ya ofisi.
* Usivae viatu vya wazi. Vaa viatu vya kawaida, hasa vinavyofunika vidole .
* Epuka kuvaa rangi zinazowaka sana, unaweza kuvaa nguo za rangi
mbalimbali, lakini zisiwe rangi zinazowaka sana. Kumbuka ; unataka watu
wakuangalie wewe na siyo rangi ya nguo yako.
Usikubali kuharibu mwonekano wako kwa sababu ya mabadiliko ya hewa,
hakikisha kabati lako lina nguo zinazokwenda na halijoto, wakati huo huo
mwonekano wako unaendelea kufanana na taaluma yako.
Imeandaliwa na Maimuna Kubegeya
Baruapepe :maikube@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment