Tuesday, December 3, 2013

12:07 PM
Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, itafanya mabadiliko makubwa katika Baraza lake Kivuli wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Bunge unaoanza leo mjini Dodoma.


Panga pangua hiyo ambayo imesukumwa na kuvuliwa nyadhifa zote kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe itawalenga pia mawaziri vivuli walioshindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zilisema Zitto ni mlengwa mkuu wa mabadiliko hayo ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu (CC) ya chama chake.

Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe iliagiza kuvuliwa nyadhifa zote, Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo kwa kile kilichodaiwa ni kukisaliti chama.

Kwa mujibu wa habari hizo, katika Mkutano wa 14 wa Bunge unaoanza leo, kambi rasmi ya upinzani imepanga kumvua rasmi Zitto nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha.

Jana, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alithibitisha kuwapo kwa mpango wa mabadiliko hayo na kwamba yanatarajiwa kufanyika kati ya mwishoni mwa wiki hii na mwanzoni mwa wiki ijayo.

Tutakaa mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo kwa sababu Kiongozi wa Kambi (Freeman Mbowe), atafika bungeni Desemba 6, mwaka huu na ndiye Mwenyekiti wa Baraza Kivuli,” alisema Lissu na kuongeza:

Mbali ya Zitto kuna Said Arfi (Mbunge wa Mpanda Mjini) ambaye amejiuzulu nafasi zake zote ikiwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Uchukuzi na tutaangalia ufanisi wa mawaziri wengine kivuli”.

Baraza kivuli linaundwa na mawaziri 18 wakiongozwa na Mbowe na Zitto aliyekuwa Naibu wake na Manaibu saba.

Kujitoa kwa wanachama

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki, alisema angeogopa kama kungekuwa na wimbi la wanachama zaidi ya 1,000 kuondoka katika chama kupinga misingi ya chama.

Lakini kama walimfuata Zitto ndani ya chama ni ruksa sisi hatuna shida lakini kama ni chama hapo kuna la kuangalia… Sisi tunaamini wanachama wetu hawafuati mtu, bali misingi,” alisema.
TOA MAONI YAKO APO CHINI:

0 comments:

Post a Comment