Thursday, December 5, 2013

3:32 AM
Katika hali ya kushangaza Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Kitila Mkumbo, amekanusha madai ya kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kupitia barua yake aliyouandikia uongozi wa chuo hicho, huku akisisitiza kuwa alijiuzulu nafasi hiyo tangu Januari 2010.

Hiyo imethibitishwa na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo- Utawala na Ofisa Mnadhimu wa Chuo Kikuu, Prof. Yunus Mgaya, iliyoeleza kuwa Dkt. Mkumbo alikanusha kimaandishi tuhuma za kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na kwamba tangu alipojiuzulu 2010, hajawahi kurejea wadhifa huo.

Wakati hayo yakiendelea Chuo hicho kimetoa taarifa ya kumsimamisha kwenye nafasi za uongozi ndani ya Chuo hicho, Dkt. Mkumbo na kuanza kuchunguzi dhidi yake, baada ya kuripotiwa kuwa anajihusisha na siasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinyume na waraka wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2000.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utawala na Ofisa Mnadhimu wa Chuo Kikuu, Prof. Yunus Mgaya,ilieleza kuwa kamati ya uchunguzi imepewa jukumu la kuchunguza na kubaini ukweli, kisha kutoa mapendekezo kwa uongozi wa chuo hicho.

“Uongozi wa Chuo utatoa uamuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,”ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya Desemba 3 mwaka huu. Chuo hicho kimewataka watu watakaohojiwa na kamati ya kumchunguza Dkt. Kitila kutoa ushirikiano wa dhati ili kubaini ukweli na kuharakisha mchakato wa uchunguzi.

Kutokana na hali hiyo, Chuo hicho kimewataka wananchi kuwa na subira kuhusiana na jambo hilo.

Taarifa hiyo, ilieleza kuwa chuo hicho kilipata taarifa kuhusu kuvuliwa uongozi Dkt. Mkumbo ndani ya CHADEMA. “Kwa mujibu wa vyombo vya habari kuwa alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA,taarifa hizo zimeushtua uongozi wa chuo kikuu, kwa sababu zimekuwa tofauti na ilivyokuwa ikieleweka kuhusu uhusiano uliokuwepo baina ya Dkt. Mkumbo na CHEDEMA,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;

“Uongozi wa chuo unapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma uliotolewa mwaka 2000 ni marufuku kwa mfanyakazi wa umma kuwa kiongozi au kuwa na madaraka yanayofanana na uongozi katika chama chochote cha siasa.”

Taarifa hiyo, ilieleza waraka huo uko wazi na wafanyakazi husika wanaufahamu na wale wanaoonesha dalili za kutetereka, ukumbushwa au kuonywa na wanaokaidi uchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

“Kwa msingi huo na kwa kuzingatia kuwa Dkt. Mkumbo hajawahi kujibainisha rasmi kama kiongozi ndani ya CHADEMA, Chuo hakikusita kumpitisha kuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu Kishiriki kuanzia mwaka jana,”Ilieleza tarifa hiyo na kuongeza kuwa kabla ya hapo Dkt. Mkumbo alikuwa Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Taaluma za Mitaala katika Shule Kuu ya Elimu Kampasi ya Mwalimu Nyerere Mlimani, mwaka 2009 hadi mwaka jana.

Chuo hicho, kimesema pamoja na wingi wa taarifa hizo za vyombo vya habari kuhusu Dkt. Mkumbo, amekanusha kimaandishi tuhuma hizo za kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na kusisitiza kuwa yeye alijiuzulu nafasi hiyo ya Ujumbe wa Kamati Kuu tangu Januari 2010. Ilielezwa kuwa Dkt. Mkumbo alifanya hivyo baada ya kuelezwa kwa sheria husika na kwamba hajawahi kurejea wadhifa huo.

Dkt. Mkumbo alivuliwa wadhifa wake ndani ya CHADEMA hivi karibuni kutokana na kudaiwa kuandaa waraka wa siri wa kufanya mapinduzi ya uongozi, ambapo tayari amepatiwa mashtaka 11 anayotakiwa kuyajibu ndani ya siku 14 na chama hicho.

Wengine waliovuliwa nyadhifa zao kwa kuhusishwa na waraka huo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Arusha, Samson Mwigamba

-Majira

0 comments:

Post a Comment