Wednesday, February 26, 2014

3:09 PM

Makongoro Nyerere

MSHITAKIWA Makongoro Nyerere anayekabiliwa na kesi ya mauaji ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imuachie huru akaishi na watoto wake au ajiue.
Makongoro alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Liwa, baada ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Inspekta Jackson Chidunda kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Makongoro, ambaye ameshitakiwa pamoja na mfanyabiashara maarufu Abubakar Marijan (50), ‘Papaa Msoffe’ aliomba mahakama imuachie huru kwa kuwa hana kesi, alikuwa anafanya kazi halali lakini ameambiwa ameua, kisa Sh milioni nane.

Makongoro Afunguka

“Tarehe nyingine kesi itakapotajwa naomba niachiwe nikakae na watoto wangu niende nikakae polisi, huko watajua pa kunipeleka kama kujiua nijiue,” aliomba Makongoro.
Hakimu Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 11, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. Aliutaka upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi. Jana Papaa Msoffe hakufika mahakamani hapo kwa madai kuwa anaumwa.


Makongoro Nyerere
Washitakiwa wanadaiwa Oktoba 11, mwaka 2011 katika eneo la Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam kwa makusudi walimuua Onesphory Kituli.
Hawakujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu na wataendelea kusota rumande kwa kuwa mashitaka yao hayana dhamana.

0 comments:

Post a Comment