Tuesday, February 25, 2014

7:33 AM

 

 Bunge la Katiba

NIMSHUKURU sana Mwenyezi Mungu kwa mara nyingine kwa kutuwezesha kuwa pamoja tena leo, tukijadili mambo muhimu ya taifa letu,

 ambalo kwa sasa lipo katika mchakato wa kupitia Rasimu ya Katiba, ambao kama utakwenda vizuri, nchi yetu itakuwa na katiba mpya wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao


Zaidi ya Watanzania wenzetu 640 wapo katika majengo ya Bunge mjini Dodoma, wakiifanya kazi hiyo muhimu kabisa, ambayo inahitaji umakini wa hali ya juu na weledi wa kutosha, vinginevyo taifa linaweza kupata kitu ambacho kitakuwa ni hasara kwa kizazi hiki na kijacho, kwani tungetegemea suala hili angalau lilete utulivu na tofauti kwa miaka mingi ijayo.

     Wajumbe hawa wa Bunge la Katiba waliokusanyika Dodoma, ndiyo wanategemewa kutupatia katiba itakayokubaliwa na makundi yote ya wananchi, kufuatia karibu kila kada kuwa na wawakilishi wao katika bunge hili maalum la Katiba.
Tanzania kama taifa, lina changamoto nyingi sana zinazozuia maendeleo yake. Wengi wamekuwa wakisema kuwa kukwama kwetu kuendelea, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na matakwa ya kikatiba. Kwamba baadhi ya sheria, zinazotokana na Katiba, zinawazuia wananchi na nchi katika maeneo mengi.

    Licha ya maendeleo, nchi yetu bado inahitaji amani na utulivu kwa kiwango kikubwa kuliko wakati mwingine wowote. Ni bunge la Katiba hili ndilo lenye wajibu wa kuangalia namna nzuri ya kuhakikisha maisha haya tuliyonayo, yanaboreshwa na ikiwa haina budi, kutungiwa sheria kali zaidi ilimradi tu watu waendelee kuishi bila kuogopa kitu ndani ya mipaka yao.
Kwa kutambua umuhimu wa bunge la katiba hili, asasi mbalimbali zilitakiwa kupendekeza majina ya watu wao, wanaodhani wanaweza kujenga hoja ya kulisaidia taifa, ili baadaye Rais afanye uteuzi kwa ajili ya kazi hii kubwa. Vyama vya siasa, asasi za kiraia, makundi mbalimbali ya kijamii, Bara na Visiwani, yalituma majina yao.

Jinsi Bunge la Katiba Lilivyo.

    Kwa jinsi Bunge la Katiba (lililochagua mzee Pandu Amir Kificho, pichani, kuwa Mwenyekiti wa Muda) lilivyo na umuhimu mkubwa, kwa vyovyote, watu waliopendekezwa na makundi yao na hatimaye kuteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, walitegemewa kuwa na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao na wenye nia njema kabisa ya kuhakikisha Watanzania zaidi ya milioni 45 wanatengenezewa mazingira ya kuishi raha mustarehe.
Lakini katika hali inayosikitisha na kukatisha tamaa, baadhi ya wajumbe hao wameonyesha udhaifu mkubwa na kuanza kutupa hofu kama kweli dhamira ya Rais Kikwete, ya kutuletea katiba mpya, inaweza kutimia kwa kiwango kilichotarajiwa.

   Inavyoonekana, wajumbe hao wamebadili nia yao ya awali ya kupigana kwa manufaa ya Watanzania, na sasa wameamua kujipigania wenyewe. Lazima niwe mkweli, nimesikitishwa sana na taarifa kwamba wenzetu hao, wanataka kupewa posho zaidi ya shilingi 300,000 ambazo hupewa kila siku tangu waliporipoti kwenye Bunge hilo maalum la Katiba kwa madai kwamba gharama za maisha zimepanda.


Kama nilivyosema mwanzo, huu ni usaliti mkubwa na aibu ya mwaka kwa wajumbe wetu. Siku zote tumekuwa tukiangushwa na watu tunaowaamini. Kama mtu anakwenda kule akifikiria kutuna kwa pochi lake, ni vipi ataweka akili zake katika hoja zinazotaka umaskini ujadiliwe na kutafutiwa mbinu za kuondolewa?




 

0 comments:

Post a Comment