Thursday, February 27, 2014

1:17 PM
Wajumbe wanawake wa Bunge Maalumu la Katiba na wageni wa jinsi hiyo watakaovaa nguo fupi ‘vimini’ au nguo za kubana, hawataruhusiwa kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge. 
 
Hayo yamo katika mapendekezo ya rasimu ya kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo, zilizowasilishwa katika semina mahsusi ya kupokea rasimu hizo, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati Maalumu, Profesa Costa Mahalu.
 
Kanuni ya 82 (9) ya mapendekezo hayo imeainisha vazi rasmi linaloruhusiwa kuwa ni vazi lolote la heshima ambalo siyo la kubana mwili, lisiloonyesha maungo.
 
Pia imeainisha mavazi yanayoruhusiwa kwa wanawake kuwa ni pamoja na gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote, suti ya kike, vazi linalovaliwa wakati wa eda na kilemba cha kadri au mtandio.
 
Kwa upande wa wanaume, mavazi rasmi ni suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na fulana.
 
Kulingana na kanuni hiyo, upande wa wanaume, pia imeainisha vazi rasmi kwa jinsia hiyo kuwa ni suti ya Kimagharibi, shati na tai, suruali ya aina yoyote isipokuwa suruali aina ya ‘jeans’.

Sehemu ya 6 ya kanuni hiyo, imeweka wazi kuwa mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu, anaweza kutoa taarifa kwenye Bunge au kwenye kamati iwapo mjumbe mwingine ataingia akiwa amevaa vazi linalovunja au kukiuka masharti ya kanuni.
 
“Mwenyekiti wa Bunge Maalum au mwenyekiti wa kamati maalumu atakaporidhika kuwa mjumbe huyo aliyetolewa taarifa hajavaa vazi rasmi, atamwamuru atoke nje ya ukumbi wa mikutano wa kamati,” inaseme sehemu ya kanuni hizo.
 
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mjumbe aliyeamriwa kutoka nje ya ukumbi, hataruhusiwa kuingia tena hadi pale atakapokwa amevaa mavazi rasmi.
 
Wakati huohuo, kamati hiyo imependekeza Bunge hilo liwe na kamati 16.
 
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana katika semina ya wajumbe wa Bunge hilo, Mwenyekiti wake, Profesa Costa Mahalu, alizitaja kamati hizo kuwa ni Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu.
 
Zingine; Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Kamati ya Uandishi, Kamati ya Maridhiano na Kamati nyingine 12.
“Kwa mpangilio huo, jumla ya kamati zote za Bunge Maalumu zinazopendekezwa na kamati hii ni 16 na majukumu ya kila kamati yameelezwa katika sehemu hiyo,” alisema Profesa Mahalu.
 
Profesa Mahalu alisema kamati yake haikufanyia marekebisho sehemu ya saba ya rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu inayoweka utaratibu wa jinsi ya kutunga masharti ya mpito na yatokanayo.
 
Alisema katika sehemu ya tisa, kamati yake imependekeza kanuni mpya inayoruhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar au Rais wa nchi nyingine yoyote kutambuliwa kama wageni. —-Mwananchi

0 comments:

Post a Comment