Wananchi wakishangilia
Mwigulu Nchemba akimuonesha aliyetobolewa jicho
Akimuonesha aliyemwagiwa tindikali
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimefanya uzinduzi rasmi
wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, huku Chifu wa
Wahehe, Abdu Sapi Mkwawa akikisuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kwa kutoa taarifa za uongo kwamba anamuunga mkono mgombea wao,
Grace Tendega.
Katika uchaguzi huo, CCM imemsimamisha Godfrey Mgimwa,
mtoto wa marehemu Dk William Mgimwa baada ya kushinda kwa kishindo kura
za maoni za chama hicho dhidi ya wagombea wengine nane.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba ndiye aliyezindua kampeni hizo zilizofanyika
katika kata ya Ifunda jimboni humo juzi.
Akishangiliwa na mamia ya wafuasi na wanachama wa chama
hicho, Mkwawa alisema “ukoo wetu una historia isiyopingika ndani ya
CCM, mimi ni kada wa CCM ninayehenzi historia hiyo na hata siku moja
siwezi kufanya vinavyotangazwa na Chadema kwenye mitandao na magazeti.”
Huku akichanganya Kiswahili na Kihehe ili aeleweke
vyema na watu wa jimbo hilo, alisema kama Chifu hakuwa na hiyana pale
mgombea wa Chadema na viongozi wa chama chake walipokwenda kumjulia hali
na kumuomba awe pamoja nao katika uzinduzi wa kampeni zao.
“Ilikuwa Februari 22 siku ambayo chama hicho kilikuwa
kinazindua kampeni zake za uchaguzi; kama ambavyo angefanya kiongozi
yoyote anayeheshimu mila za kabila lake, nami sikuwa na sababu ya
kuwakatalia, nilichofanya ni kudumisha mila kwa kuzingatia kwamba
mgombea wao ni mhehe pia” alisema.
Alisema “nafahamu kwamba uchaguzi huu ni huru na wa
kidemokrasia, nilipoombwa kupanda katika jukwaa lao sikuona tatizo pia
na nilipopewa fursa ya kuwasalimia nilisisitiza vyama vilivyosimamisha
wagombea Kalenga viendeshe kampeni zao kwa amani na utulivu na huo ndio
ujumbe ulionisukuma kupanda katika jukwaa lao.”
Alisema baada ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa
kampeni hizo kuitikia mwito wake huo aliondoka jukwaani kwa kumtaka
mgombea wao huyo aendelee na kampeni kwa amani na utulivu.
“Sikutoa baraka za kumtakia ushindi mgombea wa Chadema
kwasababu mimi ni CCM na wao wanajua hivyo, wanajua pia kwamba sina
ugomvi na chama changu; nilichowaomba ni kufanya kampeni zao kwa amani
kwasababu kama Chifu nataka kuona uchaguzi huu hauwi na machafuko,”
alisema.
Akizindua kampeni hizo, Nchemba alisema CCM imetawala
nchi hii kwa miaka 37 na hakuna mtu hata mmoja aliyeuawa katika mikutano
yake kama inavyotokea kwa Chadema.
“Katika kipindi cha miaka mitatu, watu nane wamafariki kwenye mikutano tofauti tofauti ya chama hicho,” alisema.
Akidhihirisha kwa umma wa Kalenga vurugu zinazofanywa
na chama hicho, Nchemba aliwapandisha jukwaani watu wawili, mmoja akiwa
ni yule aliyemwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa Igunga na wa
pili aliyetobolewa jicho katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kahama.
Nchemba alipongeza hekima na busara alizonazo Rais
Jakaya Kikwete akisema zinasaidia sana kuifanya nchi hii iendelee kuwa
ya utulivu na amani vinginevyo uvumilivu wa chokochoko dhidi ya CCM
usingevumilika.
Kwa masikitiko makubwa, Katibu wa CCM Wilaya ya
Mufindi, Miraji Mtaturu alionesha vibao virefu vitatu vye misumari
alivyodai vilivyowekwa na wafuasi wa Chadema katika moja ya barabara za
jimbo hilo ili kutoboa tairi za magari ya kampeni ya CCM.
“Tunawajua kwa majina wahusika wa tukio hili la
kidhalimu; na taarifa hii tumekwishawasilisha Polisi, wanaendelea
kuifanyia kazi; hii ni hatari kuendelea kushabikia chama kinachoshindwa
kuwaeleza wananchi kitawafanyia nini na badala yake kuhamsisha vurugu,”
alisema.
Akiomba kura kwa wapiga kura wa jimbo hilo, Godfrey
Mgimwa alisema “mimi sio mropokaji kama wenzetu wa Chadema, mimi ni
mtendaji, nipeni kura zenu nikamalizie kazi iliyoanza kutekelezwa na
marehemu baba yangu.”
Alisema alikuwa mshauri mkuu wa marehemu baba yake wakati wa uhai wake kwasababu ya uwezo wake mkubwa kitaaluma.
“Mimi ni mtaalamu wa biashara, masoko na fedha; na
mpaka nakuja kugombea ubunge nilikuwa mwajiriwa wa benki, kwahiyo
marehemu mzee alikuwa anaujua uwezo wangu kichwani na alikuwa akitaka
ushauri wa mara kwa mara kutoka kwangu,” alisema.
Alisema analifahamu vyema jimbo lake la Kalenga na amafanya utafiti uliomuwezesha kuyajua vyema matatizo ya wana Kalenga.
“Nipeni kura zenu zote, nazifahamu changamoto katika
sekta ya elimu, afya, maji, barabara, mawasiliano na kilimo;
nitazifanyia katika kwa kushirikiana na nyinyi kuzitatua kwa kupitia
Ilani yetu ya CCM,” alisema.
Wengine waliopata fursa ya kuhutubia mkutano huo ni
pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu na
wabunge mbalimbali wa chama hicho mkoani hapa.
Wabunge hao ni pamoja na Naibu Waziri wa Wanawake
Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa,
Leadiana Mng’ongo na Ritta Kabati na Mbunge wa Mufindi Kusini Medrad
Kigola.
0 comments:
Post a Comment