Tuesday, February 25, 2014

7:54 AM

 

Familia ya Hoyce Temu

FAMILIA ya Miss Tanzania 1999, Hoyce Nambuo Temu, inadaiwa kuingia katika mzozo mkubwa wa wapi pa kumzikia mwanafamilia mwenzao, Emmanuel Lewi Nambuo Temu (33) aliyefariki dunia Februari 15 mwaka huu katika Hospitali ya Temeke, Dar.
Mama wa marehemu Emmanuel, Hilda Lewi Nambuo ameshikilia msimamo kwamba, mwanaye akazikwe kwenye makaburi waliyozikwa mababu zao yaliyopo kwenye Kijiji cha Kikarara, Old Moshi, Kilimanjaro lakini mjomba mtu aitwaye Jacob Nambuo Temu anapinga.
Jacob na Hilda ni mtu na mdogo wake, Hilda akidaiwa kuwa mkubwa. Jacob ni mjomba wa Hoyce na Hilda ni shangazi yake.

Sakata Lafikia Mahakamani

Sakata hilo lilifikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na kupewa jalada namba 7/2014 ambapo mama wa marehemu anaitaka korti iamuru mwili wa marehemu ukazikwe huko kwa kuwa huo ndiyo wosia wa marehemu.
“Kutoruhusu mwili huo kuzikwa tunakokutaja kutaongeza uhusiano wa ugomvi wa mama wa marehemu na kaka ambaye ni mlalamikiwa,” imesema sehemu ya hati ya mahakama hiyo iliyosainiwa na Hakimu K. Mkwawa.
Mheshimiwa Mkwawa alisema kutokana na ombi la mama wa marehemu, mahakama hiyo imezuia kuchukuliwa kwa mwili huo kutoka katika Mochwari ya Hospitali ya Temeke, Dar hadi Februari 25, mwaka huu (leo) ambapo atasikiliza pande zote mbili kuhusiana na sakata hilo.
Kwa upande wake mjomba mkubwa wa marehemu, Dk. M. Nambuo Temu aliyeko nje ya nchi ametuma ujumbe akisema ameridhia marehemu akazikwe kwenye makaburi ya mababu huko Old Moshi.

Barua kwa Hoyce Temu

Katika barua yake (nakala tunayo) aliyowaandikia ndugu zake, Hoyce na Rachel Temu na wahusika wengine wa mgogoro huo, Dk. Temu alisema  amesikitika kusikia kuwa, Jacob hataki Emmanuel azikwe nyumbani kwao Old Moshi kama  yeye marehemu  alivyoagiza katika wosia wake.

“Yeye (Emmanuel) mwenyewe kabla ya kufariki dunia aliwahi kumwelezea rafiki yake Noel kuwa akifa akazikwe kwa Watemu (ukoo wa Temu) na si mahali pengine popote pale. Hatuna sababu ya kubishana juu ya mahali pa kumzika Emmanuel,” alisema Dk. Temu.
Dk. Temu alihitimisha waraka wake kwa kusema kuwa, mdogo wake (Jacob) hana haki yoyote ya kudai kuwa shamba la baba yao (marahemu mzee Temu) ni lake yeye kwa sababu hawajaligawa.

0 comments:

Post a Comment