Friday, February 28, 2014

6:22 AM
Baada ya kusota rumande kwa takribani mwaka mmoja na miezi minne, viongozi 10 wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Uamsho) jana waliachiwa kwa dhamana yenye masharti nafuu na kujumuika na familia zao.
Awali, viongozi hao walishindwa kutimiza masharti waliyopewa na mahakama ambayo yaliwataka kutoa fedha taslim Sh. milioni 25, kuwa na wadhamini watatu wakiwa ni watumishi wa serikali wenye mali isiyo hamishika ya Sh. milioni 25 pamoja na kutosafari nje ya kisiwa cha Unguja.
Hata hivyo, baada ya kilio cha washtakiwa hao wakiongozawa na mawakili wao Juma Abdallah na Salum Taufik, Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar,  Fatma Hamid Mahmoud, jana alipunguza masharti ya dhamana baada ya washtakiwa hao ambao wamekuwa wakishikiliwa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne kuanzia Oktoba 17, mwaka 2012, kulalamika kwamba masharti ya dhamana ni magumu.
Jaji huyo alikubali kila mshtakiwa kujidhamini kwa Sh. milioni 25 kwa maandishi sambamba na kuwa na wadhamini wawili badala ya watatu huku mmoja kati ya hao awe mtumishi serikali.
Kadhalika, Jaji Fatma aliwaruhusu washtakiwa hao kusafiri kwenda Pemba, lakini masharti ya kutosafiri nje ya Zanzibar pamoja na kutofanya mihadhara miskitini na nje ya misikiti yanaendelea hadi kesi ya msingi itakapoanzwa kusikilizwa.
Washtakiwa hao ni Majaliwa Fikirini Majaliwa, Faridi Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Mussa, Azani Khalid Hamdani, Suleiman Juma Suleiman,  Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmed Juma na Abdallah Said.
Washitakiwa hao walishtakiwa kwa makosa ya kufanya uchochezi, ushawishi, kuhamasisha fujo na kula njama ya kufanya kosa kulikosababisha uvunjifu wa amani na usalama wa taifa Oktoba, 2011.

Jaji Fatma alisema watuhumiwa hao wameshakaa rumande kwa muda mrefu, hivyo mahakama imetafakari na kuona kuwa dhamana ni haki ya kila mshtakiwa ambaye kosa lake linastahiki kupewa dhamana.

“Endapo mshtakiwa atakaa rumande kwa muda wa miezi minne bila ya kesi kutokuwa na ushahidi, mahakama ina uwezo wa kuifuta kesi na siyo halali kumuadhibu mtu kwa kumuweka rumande bila ya ushahidi,” alisema Jaji Fatma.
Aliwataka washtakiwa hao kuhakikisha wanalinda amani na usalama wa nchi na kwamba ikiwa watakiuka masharti hayo, mahakama itafuta dhamana waliyopewa.

 Jaji Fatma aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 27, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment