Thursday, December 5, 2013

2:58 AM
KITUNDU (Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida, Wilfred Noel Kitundu) amejiuzulu huku akinituhumu kuwa mmoja wa ‘wavamizi’ ndani ya CHADEMA ambao ndio ‘vinara’ wa migogoro ndani ya chama chetu.

Nafikiri nitasemehewa nikiweka utetezi wangu hapa jukwaani.
Kitundu ni Mwenyekiti wa muda mrefu mkoa wa Singida kupitia CHADEMA katika nchi hii.
Ni kweli kama anavyosema kwamba kwa takribani miaka 20 ya uenyekiti wake, sebule ya nyumba yake ilikuwa ndiyo ofisi ya chama ya mkoa.


Kwa maneno mengine tunaweza kusema kwamba, kwa miaka yote hiyo, chama hakikukua (katika mkoa aliouongoza).
CHADEMA haikuwa na mwenyekiti wa kitongoji, kijiji wala diwani, achilia mbali wabunge.

Ukweli ni kuwa viongozi wetu wa kwanza wa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa vitongoji na wa vijiji; walichaguliwa mwaka 2009; mwaka mmoja baada ya mimi kuvamia au kuhamia CHADEMA Singida.
Mwaka 2010 tulipata wabunge na madiwani wasiokuwa ‘maCCM’ kwa mara ya kwanza tangu Mungu aumbe mbingu na nchi.

Sitaki kujisemea sana katika hili, lakini nafikiri mchango wangu katika kuijenga CHADEMA Singida ni mdogo.
Lakini kwa upande wake, Kitundu zaidi ya kutuwekea ofisi ya mkoa sebuleni kwake, sidhani kama ametoa mchango mwingine wowote katika mafanikio haya, zaidi ya kula pesa zetu za kampeni ya udiwani katika Kata ya Urughu mwaka 2011, wakati wengine tukiwa kwenye mapambano ya uchaguzi mdogo wa Igunga.

Sidhani kama nitakuwa namsingizia mzee huyu nikisema kwamba hatujamwona akishiriki kwa maana yoyote katika harakati za kisiasa za CHADEMA Mkoa wa Singida.
Mtu aliyemwokoa kutokana na hasira ya wanachama baada ya kula hela za kampeni kata ya Urughu ni … Jaza mwenyewe!

Mwaka huo huo wa uchaguzi, kulikuwa na skendo ya mgombea ubunge wetu wa Singida Mjini kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa maelekezo ya Zitto Kabwe.
Mtu aliyetumiwa kuweka pingamizi ili mgombea wetu aenguliwe alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Singida mjini, Wazaeli Nakamia.

Tulipambana hadi tukamrudisha mgombea wetu kwa kushinda rufaa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kitundu hakuwahi kusema chochote kilichokuwa kinaendelea kwa sababu mhusika mkuu wa skendo hiyo, kama alivyo mhusika mkuu wa Mkakati wa Mapinduzi 2013 (MM), alikuwa mfadhili wake, yaani Zitto Kabwe.
CHADEMA imekuwa sana katika Mkoa wa Singida tangu 2010. Ni baada ya mimi mhamiaji (Tundu Lissu) kuvamia CHADEMA.
Naweza kusema kwamba jimbo pekee ambalo sijawahi kufanya mikutano ya hadhara ni Iramba Magharibi.
Mengine yote nimefanya mikutano ya hadhara hata kabla sijawa Mwenyekiti wa M4C Kanda ya Kati.

Kwa kifupi naweza kusema kwamba Kitundu amejiuzulu kwa sababu mfadhili wake ameng’olewa madarakani na Kamati Kuu.
Pia naweza kusema kwamba tena kwa dhamira safi, Kitundu ataondoka peke yake CHADEMA Singida. Hana mfuasi yeyote mkoa ule.

Hata mkutano wa mtaa hawezi kuitisha akapata watu. Kuondoka kwake angalau inatupunguzia mizigo ambayo tumeibeba kwa miaka mingi!
Kwa vile amemtaja marehemu Chacha Wangwe kama mmoja wa wasaliti waliong’olewa CHADEMA siku za nyuma, ni vizuri wananchi wafahamu kwamba Kitundu kama Zitto, alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ‘iliyowaaminisha’ Watanzania kwamba Chacha Wangwe alikuwa msaliti mwaka 2007.

Kama anabisha muulizeni jamaa yake anayempigania sasa hivi!
Kama ilivyo katika historia ya mapambano ya ukombozi ya zama zote, hakuna mapambano yasiyokuwa na kina Yuda Iskariote wake, yaani wale wanaosaliti kwa sababu ya vipande 30 vya fedha! Haijaanza jana wala juzi, na haitaisha kesho.

Kitu muhimu zaidi ni kwamba wasaliti wa aina hii hawajawahi kuzuia jua la haki kuchomoza na giza la ufisadi na uonevu kutoweka.
Haitakuwa tofauti kwa CHADEMA, tutashinda kama anavyosema mwanafasihi Shaffi Adam Shaffi katika kitabu chake Kuli; “Yana mwisho haya.”
Mwandishi ni Tundu Lissu
Mbunge wa Singida Mashariki.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Mwenyekiti wa M4C Kanda ya Kati

0 comments:

Post a Comment