Monday, December 2, 2013

4:27 AM


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, wamepigwa marufuku kukanyaga jijini Mwanza.

Pamoja na onyo hilo, pia viongozi hao wametakiwa kufanya kila wanaloweza ili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na wenzake waliovuliwa madaraka, warudishwe madarakani ndani ya siku nne kuanzia jana.

Kauli hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa Vijana Kanda ya Magharibi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Matawi ya CHADEMA, Mkoa wa Mwanza, Robert Gwanchele, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Gwanchele, yeye na wenzake wamelazimika kuchukua uamuzi huo kwa kuwa wanapinga kitendo cha kuvuliwa madaraka kwa viongozi hao kwa kuwa kilifanyika kinyume cha Katiba ya chama hicho.

“Pamoja na kuwapiga marufuku kukanyaga mkoani Mwanza viongozi hao wa kitaifa, kama Zitto, Dk. Mkumbo Kitila pamoja na Samson Mwigamba wasiporejeshwa madarakani, hadi Desemba 4 mwaka huu, vijana Kanda ya Magharibi tutaandaa maandamano yasiyo na ukomo kushinikiza Dk. Slaa na Mbowe wajiuzuru ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

“Chadema tumeingiliwa na mdudu aitwae ubinafsi kwani kuna baadhi ya viongozi wa chama ni makuwadi wa viongozi wetu wa ngazi za juu kufanya wanayotaka bila kuchukuliwa hatua.

“Chadema ni chama kinachojali watu wa upande fulani wa nchi, hivi viongozi kama Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) pamoja na Kileo ambao waliamua kumshambulia Zitto kupitia mitandao ya kijamii wamechukuliwa hatua gani na chama?.

“Tutahakikisha tunawaondoa viongozi wote wa ngazi za juu kwa nguvu ya umma kwani Chadema sio mali ya mtu binafsi, chama hiki nicha wanachama.

“Hatutaki kuyumbishwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi, hao wanapaswa kukaa pembeni kwanza kupisha uchunguzi na kama hawataki kupisha nguvu ya umma itawaondoa na ndio maana sisi vijana wa Kanda ya Magharibi, tumeamua kuwapiga marufuku Mbowe na Dk. Slaa wasikanyage Mwanza kwani wao tayari wameamua kujijengea himaya yao isiyoguswa katika mikoa ya kaskazini, sasa Mwanza wanakuja kutafuta nini.

“Mbowe na Dk. Slaa ni watuhumiwa hawapaswi kuendelea kuwa viongozi wa Chadema, hao wanapaswa kujiondoa ili nao wachunguzwe juu ya matumizi mabaya ya fedha za chama,” alisema Gwanchele.

Pamoja na kuwashambulia Mbowe na Dk. Slaa, Gwanchele pia aliwarushia kombora wabunge wa Chadema wanaotoka Mkoa wa Mwanza kwa kile alichosema nao wameshiriki katika kuvuliwa madaraka kwa Zitto, Dk. Kitila na Mwigamba.

Kutokana na hali hiyo, alisema wabunge hao, Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiel Wenje (Nyamagana) na Salvatory Machemli (Ukerewe), wamepoteza uhalali wa kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Mwanza.

“Wabunge wa chadema Mkoa wa Mwanza hivi sasa wanajiona wako juu ya chama na wamekuwa wakitoa matamko ya kuunga mkono kuondolewa kwa Zitto na wenzake wakati sisi wananchi hatukuwatuma kufanya hayo.

“Kwa hiyo, nao wanapaswa kuondolewa madarakani mara moja kwa usaliti wao kwa wapiga kura wao,”alisema.


TOA MAONI YAKO APO CHINI

0 comments:

Post a Comment