Tuesday, January 14, 2014

3:11 AM

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema anamsubiri Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe mahakamani.


 Zitto ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mbowe kutangaza kumburuza mahakamani, kutokana na kile kinachodaiwa kumzushia tuhuma za uongo. “Nasema sitaki malumbano na kiongozi yeyote, nachotambua masuala ya mahakamani yanajibiwa mahakamani na si vinginevyo,” alisema Zitto.

Zitto alitoa kauli hiyo, baada ya MTANZANIA kutaka kujua msimamo wake kutokana na kauli ya Mbowe kukusudia kumshitaki, kutokana na madai ya kusema uongo dhidi yake.

Zitto ambaye yuko nchini Nigeria anakohudhuria vikao vya Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali kwa nchi za Afrika, alisema pamoja na hali hiyo, mahakama ndiyo njia pekee ambayo haki ya mtu inaweza kupatikana.
 

Alisema kwa msingi huo, hivi sasa hayuko tayari kuruhusu malumbano ambayo hayana tija kwa taifa.

“Nipo Nigeria na bahati mbaya ninaumwa sana, ila hivi leo ninamshukuru Mungu nimepata nafuu kidogo. Kama nilivyosema mwanzo sitaki malumbano na mtu.

Pamoja na kusema anaumwa, hakuwa tayari kufafanua ni ugonjwa gani unaomsumbua.

“Huu muda nahitaji kutafakari maisha yangu kisiasa na kwa vyovyote vile masuala ya mahakamani yatajibiwa mahakamani,” alisisitiza Zitto.

Juzi Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya CHADEMA, ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kusema, Mbowe amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote, zikilenga kumchafua kwa nafasi yake ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza.

Kutokana na hali hiyo, tayari Mbowe kwa mujibu wa taarifa hiyo, ameshawasiliana na wanasheria wake kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya aliyezusha uongo huo.

Ingawa taarifa hiyo haikutaja jina la Zitto, lakini hivi karibuni mbunge huyo katika ukurasa wake wa facebook, aliibua tuhuma nzito dhidi ya Mbowe.

Zitto, Samson Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo, walivuliwa nyadhifa zao na Kamati Kuu (CC).

Baadaye CC iliwatimua uanachama, Mwigamba na Kitila kwa tuhuma za kukisaliti na kukihujumu chama, huku Zitto akikimbilia mahakamani kuzuia asijadiliwe.

Katika tuhuma hizo, Zitto alidai Mbowe alipokea michango ya fedha kutoka kwa makada wa CCM, Nimrod Mkono na Rostam Aziz, kusaidia kampeni za CHADEMA mwaka 2005 na 2010.

Pia Zitto, alidai Mbowe alipokea Sh milioni 40 mwaka 2005 kutoka kwa Mkono ili asifanye kampeni katika Jimbo la Musoma Vijijini, na kwamba mwaka 2008 alimpatia Sh milioni 20 kusaidia CHADEMA ishinde uchaguzi mdogo wa Tarime.

Kutokana na tuhuma hizo, CHADEMA kupitia Ofisa Habari Mwandamizi, Tumaini Makene, iliamua kujibu mapigo.

Katika taarifa hiyo, ilieleza tuhuma hizo ni moja ya mikakati ya Zitto na wenzake wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama.

“Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe, amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote, zikilenga kumchafua kwa nafasi yake.

“Tuhuma hizo ni pamoja na kwamba, Mbowe mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka kwa Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono kiasi cha Sh milioni 40 ili Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.

“Mwaka 2008, Mbunge Mkono alimpatia Mbowe Sh milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama mkopo na akalipwa.”

Zitto alidai mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mkono alimpatia Mbowe Sh milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais, huku akipokea Sh milioni 100 kutoka kwa Rostam.

Kutokana na hali hiyo, Idara ya Habari ya CHADEMA, ilisema kupitia taarifa yake kuwa hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo, bali ni uongo na uzushi uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM.

0 comments:

Post a Comment